Chimano kuzindua kibao kipya

Marion Bosire
2 Min Read

Willis Austin Chimano mmoja wa wanachama wa iliyokuwa bendi ya Sauti Sol ametangaza kwamba anapanga kuzindua kibao kipya, katika kile anachokirejelea kuwa safari mpya ya maisha yake.

Kupitia akaunti yake ya Instagram, Chimano amefichua kwamba wimbo huo kwa jina “Do You Remember” utatoka rasmi Agosti 9, 2024.

Safari mpya ya maisha yake anasema imeanza baada ya kutimiza umri wa miaka 37.

“Nina wingi wa shukrani kwa umbali huu ambao maisha yamenifikisha. Nimeishi kwa miaka 37. Maisha yangu ya awali yalinitambulisha na kunijaza lakini kama sura iliyosomwa, tulimaliza kusoma na ni wakati wa kufungua ukurasa mpya.” aliandika Chimano.

Chimano aliendelea kuelezea kwamba anashukuru kwa kuweza kushiriki kipaji cha sauti yake na mashabiki zake na sasa ni fursa ya kujenga jamii na kuinuana.

Kuhusu uanachama wake katika bendi iliyovunjwa ya Sauti Sol, Chimano anashukuru kwa kuweza kufanya kazi humo anapoangazia safari ya muziki kama mwimbaji huru.

Kando na “Do You Remember” Chimano amesema kwamba anapanga kutoa miziki mingi mwaka huu akijirejelea kuwa msanii mpya.

Bendi ya Sauti Sol ilivunjwa mwaka 2023 baada ya kuwepo kwa miaka 18 na wanachama wake wakaangazia kazi zao binafsi.

Mwanzo wa mwaka huu mmoja wa wana Sauti Sol kwa jina Savara Mudigi alihojiwa na kuelezea kwamba hawakuwa wanasambaratisha bendi ila wanachukua muda kufanya kazi kando kando kama njia ya kuchochea ubunifu zaidi.

Share This Article