Mshindi wa nishani ya fedha ya Olimpiki Timothy Cheruiyot na bingwa wa Afrika Brian Komen wamefuzu kwa fainali ya mita 1500 katika michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.
Komen amemaliza wa nne kwenye semi fainali ya Jumapli usiku akitimka kwa dakika 3 sekunde 32.57 katika mchujo wa kwanza.
Mchujo huo uliongozwa na bingwa mtetezi Yakob Ingebrigsten wa Norway aliyetumia dakika 3 sekunde 32.38.
Reynold Kipkorir aliambulia nafasi ya 10 katika mchujo huo wa kwanza na kukosa tiketi ya fainali.
Cheruiyot aliyenyakua nishani ya fedha miaka mitatu iliyopita jijini Tokyo nchini Japani, alijikatia tiketi kwa fainali ya Jumanne ijayo baada ya kumaliza wa tano katika nusu fainali ya pili.
Cheruiyot alitumia dakika 3 sekunde 32.30 kukamilisha nusu fainali ya pili iliyoshindwa na Yared Nuguse wa Marekani kwa dakika 3 sekunde 31.72.