Waliokuwa Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC Juliana Cherera na Irene Masit wameelezea masaibu waliokumbana nayo baada ya kujiuzulu nyadhifa zao kwenye tume hiyo.
Wanasema hali imekuwa ngumu kwao tangu walipojiuzulu kiasi cha kuhangaika kujikimu kimaisha na wao wenyewe na familia zao kutishiwa.
Cherera ambaye alikuwa Naibu Mwenyekiti wa IEBC alijiuzulu wadhifa huo baada ya kushinikizwa kufanya hivyo baada ya kujitenga na matokeo ya urais ya mwaka 2022.
Wengine waliojiuzulu ni makamishna Justus Nyang’aya na Francis Wanderi waliofika mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo inayoongozwa na Kalonzo Musyoka na Kimani Ichung’wah.
Hata hivyo, Masit aliamua kujitetea mbele ya jopo lililoonggozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule lililompata na hatia na hivyo kusababisha kutimuliwa kwake.
“Hali imekuwa mbaya kwetu na familia zetu. Bado nina familia changa na mtoto wangu wa mwisho ana umri wa miaka 7. Hali si salama kwetu. Tulitishiwa kwa sababu ya tulichokijua. Tumepitia mengi, tulijiuzulu kwa sababu ya kushinikizwa,” alisema Cherera wakati akizungumza mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano kwa njia ya video.
Cherera anasema kuna haja ya kuufanyia ukaguzi uchaguzi wa urais wa mwaka 2022 ili kubaini kilichojiri kwa manufaa ya nchi akidai matokeo yake yalijumulishwa na watu wachache na hayakuthibitishwa.
Huku aksikika kuwa mwenye hofu tele, Masit alisema alivyotishiwa kiasi cha kukimbilia nje ya nchi kwa sababu ya usalama wake.
“Ilibidi nichukue pikipiki na kuelekea uwanja wa ndege haraka na kukimbilia nje ya nchi kwa sababu ya usalama wangu. Sijawahi kukanyaga nyumbani kwangu katika Bonde la Ufa kwa sababu ya kutishiwa na kulaumiwa kuwa niliisaliti jamii yangu,” alisema Masit.
“Napitia wakati mgumu, hata kujikimu kimaisha ughaibuni imekuwa vigumu.”
Makamishna hao wanne wa zamani wa IEBC, maarufu kama “Cherera Four” wanashikilia msimamo kuwa uchaguzi wa urais wa mwaka 2022 haukuwa wa uwazi na kamwe hawakuikodolea macho fomu namba 34C ambayo huwa na matokeo ya urais.
Walimlaumu aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya IEBC Wafula Chebukati kwa kuwatenga katika mchakato wa ujumulishaji kura za urais wakiitaja hatua hiyo kuwa kinyume cha sheria.
Chebukati pamoja na waliokuwa makamishna Prof. Abdi Guliye na Boya Molu wamesema hawatafika mbele ya kamati hiyo kuzungumzia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 wakisema utata kuuhusu ulisuluhishwa na Mahakama ya Juu.