Chepkoech ashinda mita 5,000 Nyayo

Tom Mathinji
2 Min Read

Mshikilizi wa rekodi ya dunia na mshindi wa nishani ya shaba ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na kidimbwi cha maji Beatrice Chepkoech ameibuka mshindi wa mita 5,000 katika siku ya pili ya mkondo wa tatu wa mbio za chama cha Riadha katika uwanja wa taifa wa Nyayo.

Chepkoech anayeangazia kujizoa katika michezo ya Olimpiki ya mwaka huu jijini Paris Ufaransa alizikamilisha mbio hizo kwa kutumia muda wa dakika 15 sekunde 22 nukta 02.

Rebecca Njeri wa Central alimaliza wa pili kwa dakika 15 sekunde 52 nukta 91, huku Vivian Jebiwott, akiambulia nafasi ya tatu kwa dakika 16 sekunde 46 nukta 08.

Katika fainali ya kwanza ya mita 800,Koitatoi Kidali alishinda fainali ya kwanza ya mita 800 kwa muda wa dakika 1 sekunde 46 nukta 66,akifuatwa na Alfred Kipketer kwa dakika 1 sekunde 46 nukta 86 huku Lenny Lemashon akimaliza wa tatu.

Fainali ya pili ya mita 800 ilishindwa na Alex Ngeno kwa dakika 1 sekunde 46 nukta 83 ,akifuatwa na Cornelius Tuwei kwa dakika 1 sekunde 47 nukta 35 naye Vincent Keter akaridhia nafasi ya tatu kwa dakika 1 sekunde 47 nukta 43.

Wanariadha wengi walitumia mashindano hayo kujiandaa kwa msimu mpya na pia majaribioi ya kitaifa ya kufuzu kwa michezo ya Afrika yatakayoandaliwa uwanja wa Nyayo mwezi ujao.

Website |  + posts
Share This Article