Waziri wa ushirika na ustawi wa biashara ndogo na zile za kadri Simon Chelugui, amepuuzilia mbali madai kuwa kampuni ya maziwa ya New KCC ni miongoni mwa zile zitabinafsishwa.
Aidha Waziri huyo alidokeza kuwa kampuni hiyo itaboreshwa na serikali, kwa kuwa huwafaidi pakubwa wakulima wengi kwa kununua bidhaa zao
Kulingana na Chelugui, Kuna agizo la baraza la mawaziri la miaka minne, linalozuia kubinafsishwa kwa kampuni hiyo.
“ Mnamo tarehe 29 mwezi Machi mwaka 2019, baraza la mawaziri liliazimia kuiondoa kampuni ya New KCC kutoka orodha ya mpango wa ubinafsishaji. Azimio hilo hadi sasa lingalipo na litatolewa tu na azimio lingine la baraza la mawaziri,” alisema Waziri Chelugui.
Waziri huyo alisema ataandikia hazina kuu akinukuu Azimio hilo la mwaka 2019. Katika barua hiyo, Chelugui alisema atatoa sababu kwanini baraza la mawaziri la wakati huo lilisema kampuni hiyo haita binafsishwa.
Hata hivyo Kulingana na Chelugui, ikiwa kampuni ya New KCC itabinafsishwa, wakulima watapewa kipaunbele kupitia mashirika yao.
Waziri huyo aliyasema hayo, aliposhiriki meza ya mazungumzo na bodi ya usimamizi ya kampuni ya New KCC, kujadili mipango mipya ya kimkakati ya kampuni hiyo.