Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga ametishia kuitisha tena maandamano mwaka huu ikiwa utawala wa Kenya Kwanza hautabatilisha sheria ya fedha ya mwaka 2023 na kupunguza gharama ya juu ya maisha inayowahangaisha Wakenya.
Upinzani umekuwa ukiisuta serikali ya Rais William Ruto kwa kile unachotaja kuwa hulka ya kuongeza ushuru ambao umefanya maisha kuwa magumu zaidi.
Wanaazimio wanasema ni sharti mfumo wa ushuru wa Kenya Kwanza upitiwe upya la sivyo wapulize tena kipenga cha maandamano.
Matamshi ambayo Rais William Ruto, akizungumza huko Nyandarua jana Jumanne, aliyapuuzilia mbali akiutaka upinzani kutoa mpango mbadala unaotaka utekelezwe badala ya kujigamba kwa maneno matupu.
Kulingana na Ruto, matatizo yanayoikumba nchi ya Kenya hayatokani na ushuru kamwe.
“Shida ya Kenya si ushuru, shida ya Kenya ni madeni,” Ruto aliuambia upinzani.
“Badala ya kuwasumbua wananchi kwa kuleta fujo na kuleta vita, ambieni hawa wananchi mpango wenu tofauti na wetu ni gani? Sisi tumesema tunataka tulipe ushuru, tuokoe Kenya kwa madeni. Nyinyi mtuambie yenu ni gani? Msituambie ati mnapanga vita?”
Mwaka jana, muungano wa Azimio uliitisha maandamano ya kupinga kutekelezwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023 na kuitaka serikali kupunguza gharama ya juu ya maisha.
Hata hivyo, maandamano hayo yalikuwa chanzo cha umwagikaji damu huku watu kadhaa wakiuawa katika makabiliano na maafisa wa usalama huku wengine wengi wakijeruhiwa.
Hali ilipokuwa si hali, kamati ya uwiano wa taifa iliundwa kuangazia malalamishi ya upinzani.
Kamati hiyo iliongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah.
Hata hivyo, ripoti ya kamati hiyo imesababisha migawanyiko katika muungano wa Azimio huku viongozi kadhaa kama vile kiongozi wa chama cha Narc-K Martha Karua na yule wa DAP-K Eugene Wamalwa wakiipuzilia mbali.
Wanadai ripoti hiyo haikuangazia suala kuu la gharama ya maisha linalowazonga Wakenya.
Huku kukiwa na migawanyiko hiyo, mustakabali wa ripoti hiyo bado haujulikani.