Chebukati: Hatutafika mbele ya kamati kuzungumzia masuala yaliyosuluhishwa

Martin Mwanje
3 Min Read

Aliyekuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC Wafula Chebukati hatafika mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo kuzungumzia uchaguzi wa mwaka 2022. 

Aidha waliokuwa makamisha wa tume hiyo Prof. Abdi Guliye na Boya Molu hawatafika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah.

Kupitia barua waliotumiwa Septemba 25, 2023, watatu hao walikuwa wametakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ili kuzungumzia baadhi au masuala yote matano yanayojadiliwa.

“Tumepitia masuala matano yanayojadiliwa na tungependa kuwataarifu kuwa hatungependa kuzungumzia lolote mbele ya kamati hiyo,” walisema Chebukati, Prof. Guliye na Molu katika taarifa ya pamoja.

“Uamuzi wetu umetokana na mtazamo kwamba masuala yanayoangaziwa na kamati hiyo yapo chini ya mamlaka ya taasisi zetu au tayari yamesuluhishwa na taasisi zilizobuniwa kisheria kuyashughulikia.”

Wanatoa mfano wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 hususan utata uliozingira uchaguzi wa urais na ambao wanasema tayari umesuluhishwa na Mahakama ya Juu.

“Wakati wa muhula wetu afisini, tulitekeleza majukumu yetu, ikiwa ni kuendesha kwa mafanikio uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Ni kupitia uchaguzi huo ambapo Rais, Magavana, Maseneta, Wabunge na Wawakilishi Wadi walishika hatamu za uongozi. Baadhi yao sasa ni wanachama wa kamati hii. Utendakazi wetu kwa mujibu wa sheria kama ambavyo tumeelezea ni dhahiri,” alisema Chebukati na wenzake.

Isitoshe, wanasema kushiriki kwao katika mazungumzo hayo itakuwa sawia na kusaliti wafanyakazi wa IEBC walionyanyaswa na kuuawa na itakuwa tuzo kwa wanaopenda kuvunja sheria.

Badala yake, watatu hao sasa wanapendekeza kubuniwa kwa Tume ya Uchunguzi ili iichunguze matukio yaliyojiri katika ukumbi wa Bomas Agosti 15, 2022, matukio wanayosema yaliiharibia nchi sifa.

Siku hiyo, baadhi ya viongozi wa Azimio walizua rabsha wakipinga juhudi za Chebukati kutangaza matokeo ya urais waliodai yalikuwa ya kutilia shaka.

Hatimaye, Chebukati alitangaza matokeo hayo baada ya hali ya vuta ni kuvute na maafisa wa polisi kuingilia kati na kutuliza hali.

Makundi kadhaa yamekuwa yakifika mbele ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusiana na masuala matano yanayojadiliwa na kamati hiyo.

 

Share This Article