Chebukati asema mapinduzi ni tishio kwa demokrasia

Marion Bosire
2 Min Read

Aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini IEBC Wafula Chebukati amesema kwamba mapinduzi ya serikali za nchi kadhaa barani Afrika yanayotekelezwa na wanajeshi tishio kwa mazuri yaliyoafikiwa kupitia demokrasia.

Chebukati anahisi mapinduzi yanasabishwa na ukosefu wa uwazi katika mifumo ya uchaguzi.

Matamshi ya Chebukati yanajiri saa chache tu baada ya jeshi la nchi ya Gabon kupindua serikali punde baada ya majibu ya uchaguzi mkuu kutangazwa ambapo Rais Ali Bongo alitangazwa mshindi. Familia ya Bongo imeongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 50.

Wanajeshi hao walitoa hotuba kupitia kituo cha runinga ambapo walisema wametupilia mbali majibu ya uchaguzi uliofanywa Jumamosi. Walimtangaza Jenerali Brice Oligui Nguema kuwa kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo ya Gabon.

Mwezi Julai mwaka huu, Rais wa Niger Mohamed Bazoum alibanduliwa madarakani na wanajeshi baada ya hali sawia kushuhudiwa katika nchi za eneo la magharibi mwa Afrika kama Burkina Faso, Guinea na Mali.

Kulingana na Chebukati, hali katika nchi husika ingekuwa tofauti kabisa iwapo mifumo ya uchaguzi ingekuwa na uwazi kwa kujumuisha waangalizi. Anasema waangalizi ni muhimu kwa sababu wanachangia katika kuafikia uwazi.

Maoni ya mwenyekiti huyo wa zamani wa tume ya uchaguzi yanajiri wakati ambapo kamati ya mazungumzo ya kitaifa inapanga kujadili uchaguzi wa urais ambao alisimamia. Upande wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya unahisi kwamba kinara wake Raila Odinga alishinda kwenye uchaguzi huo.

Share This Article