Chebet na Obiri walenga kuhifadhi Boston Marathon

Dismas Otuke
2 Min Read

Evans Chebet  na Hellen Obiri watalenga kuhifadhi mataji ya mbio za Boston Marathon katika makala ya 128 yatakayoandaliwa Jumatatu April  15.

Chebet ambaye ameshinda mbio hizo mara mbili mtawalia atawania  kuwa mwanariadha wa  kwanza kutwaa ushindi mara tatu kwa mpigo baada ya miaka 16 na wa tano kwa jumla kuafikia matokeo hayo tangu Mkenya Robert Cheruiyot mwaka 2006.

Wakenya wengine katika mbio za wanaume ni Cybrian Kotut,John Korir aliyemaliza wa tisa mwaka 2023  na Albert Korir aliyemaliza wa nne mwaka uliopita.

Hata hivyo Chebet anakabiliwa na wakati mgumu kutetea tajihiyo kwani hajakimbia tangu ashinde makala ya mwaka jana,akitatizwa na majeraha ya muda mrefu.

Upinzani kwa Wakenya hao watatu utatoka kwa bingwa wa Valencia marathon Sisay Lemma,bingwa wa London marathon mwaka 2020 Shur Kitata ,Haftu Teklu na Mohammed Esa wote kutoka Ethiopia,Gabriel Geay wa Tanzania na Wamarekani Sam Chelanga na Elkanah Kibet.

Obiri aliyeandikisha historia kuwa mwanamke wa kwanza kutwaa ubingwa wa Boston na New York marathon mwaka jana tangu mwaka 1989,atakuwa akitetea taji ya vipusa dhidi ya washiriki wengine wanane wanaojivunia muda wa chini ya saa 2 na dakika 20.

Obiri atakabiliana na bingwa wa New York marathon mwaka 2022 Sharon Lokedi,mshindi wa nishani ya fedha ya dunia mwaka 2022 Judith Korir,Edna Kiplagat,Mary Ngugi na Hellah Kiprop.

Obiri anapania kuandikisha historia kuwa mwanariadha wa kwanza kutoka Kenya kwa upande wanawake kuhifadhi taji hiyo tangu Catherine  Ndereba kufanya hivyo mwaka  2004 na 2005.

Share This Article