Mashambulizi ya wanamgambo na ukosefu wa uaminifu unaotokana na taarifa za upotoshaji vinazuia mapambano ya kuangamiza ugonjwa wa polio nchini Pakistan.
Hata hivyo, timu za wafanyakazi wa kujitolea zinajibidiisha kutoa chanjo hiyo.
Pakistan na Afghanistan ndio nchi pekee ambako ugonjwa huo unaosababishwa na virusi bado unaenea.
Ugonjwa huo hasa huathiri watoto na mara nyingine kusababisha kupooza kipindi chote cha maisha.
Visa vya polio nchini Pakistan vinaongezeka huku visa 45 vikiripotiwa kufikia sasa mwaka huu. Idadi hiyo imeongezeka kwa visa 6 ikilinganishwa na mwaka wa 2023 na kisa kimoja pekee mwaka 2021.
Ugonjwa wa polio unaweza ukazuiwa kwa urahisi kwa kutoa chanjo ya vitone vichache, lakini katika baadhi ya maeneo ya Pakistan, wafanyakazi wanahatarsha maisha yao kuwaokoa watu wengine.
Wiki jana, watu 7 wakiwemo watoto waliuawa wakati bomu lilipolenga polisi waliokuwa wakisafiri kwenda kutoa ulinzi kwa wafanyakazi wanaotoa chanjo. Siku moja kabla, maafisa wawili wa polisi waliuawa na wanamgambo.
“Wakati tunaposikia timu ya utoaji chanjo dhidi ya polio imeshambuliwa, inatuhuzunisha sana,” alisema mfanyakazi wa afya Zainab Sultan, mwenye urmri wa miaka 28, wakati akizuru nyumba hadi nyumba kutoa chanjo katika eneo la Panam Dehri kaskazini mashariki mwa Pakistan.
“Wajibu wetu kwa sasa ni kuendelea na kazi yetu. Kazi yetu ni kulinda watu dhidi ya ulemavu na kufanya kuwa wanachama wenye afya katika jamii.”