Mkuu wa Trafiki katika kaunti ya Nairobi Joseph Chirchir ametangaza kuwa barabara kadhaa zitafungwa keshokutwa Jumapili, siku ambayo timu ya taifa Harambee Stars itafungua dimba la CHAN 2024 kwa kuchuana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC katika Uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi Sports Centre, Kasarani.
Kwa misingi hiyo, waendeshaji magari wametakiwa kupanga vyema ratiba ya safari zao ili wasije wakahangaika siku hiyo.
Kulingana na Chirchir, miongoni mwa barabara zitakazofungwa ni ile ya Aerodrome kuanzia mzunguko wa barabara wa Madaraka hadi mzunguko wa barabara ya Bunyala, sehemu ya barabara ya Lang’ata kati ya mizunguko ya barabara ya Madaraka na Lusaka.
Ameongeza kuwa sehemu ya barabara ya Mombasa, kati ya mzunguko wa Lusaka na Bunyala itafungwa upande mmoja.
Matatu za abiria zinazoelekea Kasarani zimeshauriwa kutumia barabara ya Ruaraka Baba-Dogo na Ngomongo kuelekea mzunguko wa barabara ya Ngomongo.
Wenye magari kutoka barabara Thika wametakiwa kutumia aidha easten Bypass, barabara ya Kiambu au ile ya Limuru.