Wapiga kura nchini Botswana wamekikataa chama tawala cha muda mrefu cha nchi hiyo katika matokeo ambayo yanaashiria mtikisiko wa kisiasa katika taifa hilo lenye utajiri wa almasi kusini mwa Afrika.
Chama cha Kidemokrasia cha Botswana (BDP) kilichokuwa madarakani tangu uhuru mwaka 1966 kilikuwa kimeshinda kiti kimoja tu cha ubunge kufikia mapema Ijumaa asubuhi, matokeo ya awali ya uchaguzi yanaonyesha.
Chama cha Umbrella for Democratic Change (UDC), kinachoongozwa na wakili wa haki za binadamu Duma Boko, kilishinda viti 20, kulingana na hesabu za awali.
UDC kinaonekana kitaunda serikali huku kikitarajiwa kupitisha kizingiti cha viti 31 kwa wingi wa wabunge.
Wabunge wanapomchagua rais nchini Botswana, Duma Boko yuko mbioni kuwa mkuu wa nchi mara tu bunge litakapokutana kwa mara ya kwanza.
Boko, ambaye anagombea kwa mara ya tatu, amewataka wafuasi wake “kudumisha umakini na nidhamu”.
Licha ya kusimamia mabadiliko makubwa nchini Botswana, ukuaji duni wa uchumi wa hivi karibuni na ukosefu mkubwa wa ajira ulidhoofisha umaarufu wa BDP.
Atachukua nafasi ya Mokgweetsi Masisi ambaye aliingia madarakani tangu 2018 na kuongoza kampeni ya BDP iliyoshindwa kupata matokeo mazuri ya kura.
Katika kampeni yake Rais alinadi ujumbe kwamba chama chake kinaweza kuleta “mabadiliko”, lakini hakuna wapiga kura wa kutosha waliokuwa na imani kwamba BDP knaweza kufanya kile ambacho nchi inakihitaji.