Chama cha Farmers chatoa ilani ya kujiondoa Kenya Kwanza

Tom Mathinji
1 Min Read
Chama cha Farmers chatoa ilani ya kujiondoa katika Muungano wa Kenya Kwanza.

Chama cha Farmers kimetoa ilani ya siku 30 ya kujiondoa katika muungano wa Kenya kwanza, kikitaja kukiukwa kwa mkataba wa maelewano kati ya pande husika.

Kupitia kwa taarifa leo Jumanne, Katibu Mkuu wa chama hicho Simon Kamangu, alisema hatua hiyo imeafikiwa baada ya muungano wa Kenya Kwanza na chama cha ODM kubuni serikali jumuishi kupitia Mkataba wa Maelewano, bila mashaurino na vyama tanzu, chama cha Farmers kikiwemo.

“Baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya Kitaifa Aprili 7, 2025, Chama cha Farmers kinatoa ilani ya siku 30 kujiondoa katika muunagno wa Kenya Kwanza kuambatana na sehemu ya 8 ya Mkataba wa Maelewano,’ alisema Kamangu.

Kamangu aliongeza kuwa,”Hatua ya Kenya Kwanza kubuni serikali jumuishi na ODM, inahujumu uwazi, ujumuishaji na heshima baina ya pande husika”.

Chama cha Farmers kilisema kiliingia katika muungano na Kenya Kwanza  Machi 23, 2022, kikitarajia wanachama wake, wengi wao wakiwa wakulima, watanufaika pakubwa.

Hiki ni chama pili kutoa ilani ya kujiondoa muungano wa Kenya Kwanza baada ya kile cha DP kutoa ilani sawia.

Chama cha DP kinahusishwa na Waziri wa Utumishi wa Umma wa zamani Justin Muturi ambaye alipigwa kalamu kutoka kwenye wadhifa huo siku chache zilizopita.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article