Raia wa Chad wameamkia shughuli ya kupiga kura mapema Jumatatu kumchagua Rais mpya miaka mitatu, tangu kupinduliwa kwa serikali ya nchi hiyo huku Mahamat Idris Deby akitwaa mamlaka.
Kulingana na wadadisi Mahamat Deby aliyetwaa mamlaka baada ya waasi kumuua babake Idriss Deby Aprili mwaka 2021,anapigiwa upato kuibuka mshindi.
Wapiga kura milioni 8.5 wamejisajili kwa zoezi hilo ambalo matokeo yake yamekisiwa kuanza Mei 21, huku matokeo rasmi yakitanzwa kufikia Juni 5.
Mshindi wa Urais ni sharti apate uungwaji mkono wa zaidi ya asilimia 50, la sivyo kura za marudio zitaandaliwa Juni 22.
Hata hivyo upinzani tayari umeelezea hofu ya wizi wa kura hususan kufuatia mauaji ya Yaya Dillo aliyetarajiwa kumpinga Deby Februari 28.