Mabingwa mara tano wa Afrika,Cameroon na Namibia walijikatia tiketi kwa makala ya 34 ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika yatkayoandaliwa kati ya Januari 13 na Februari 11 mwaka ujao nchini Ivory Coast.
Indomitable Lions waliwahi tiketi baada ya kuwatitiga Burundi mabao matatu kwa bila katika mechi ya mwisho ya kundi C Jumanne usiku, Bryan Mbeumo,Christopher Wooh na nahodha Vincent Abubakar walipachika goli moja kila mmoja uwanjani Raumde Adjia mjini Garroua.
Cameroon wanaonozwa na mchezaji wa zamani Rigibert Song waliongoza kundi C kwa pointi 7 ,mbili zaidi ya Namibia waliomaliza wa pili huku timu zote zikijikatia tiketi kwa kipute cha mwakani.
Idadi kamili ya mataifa 24 yatakayoshiriki patashika hiyo imekamilika kufuatia kumalizika kwa mechi za makundi za kufuzu na kinachosubiriwa ni droo itakayoandaliwa mjini Abidjan Ivory Coast Oktoba 12 ambapo kila mmoja atabaini wapinzani wake.
Kati ya timu zilizofuzu 12 ni mabingwa wa zamani wa Afrika wakati Tanzania na Gambia wakishiriki kwa mara ya pili kila moja.
Hata hivyo hakutakuwa na timu iiliyofuzu kipute hichao kwa mara ya kwanza nchini Ivory Coast.
Timu zilizofuzu ni :-Ivory Coast wakiwa wenyeji,Algeria, Angola, Burkina Faso, Cameroon, Cape Verde, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo , Misri, Equatorial Guinea, The Gambia, Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Mali, Mauritania, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Senegal,Afrika Kusini, Tanzania, Tunisia na Zambia.
Senegal ndio mabingwa watetezi baada ya kuwashinda mabingwa mara saba Misri mwaka 2022.