CAK yaitoza supamaketi ya Carrefour faini ya shilingi bilioni 1.1

Martin Mwanje
2 Min Read

Mamlaka ya Ushindani Nchini Kenya, CAK imeitoza supamaketi ya Carrefour faini ya shilingi bilioni 1.1 kutokana na utumiaji mbaya wa uwezo wake wa kufanya manunuzi dhidi ya kampuni za Pwani Oil na Woodlands zinazoisambazia bidhaa.

Kampuni ya Woodlands huchakata na kuziuzia supamaketi asali kutoka kaunti ya Kitui.

Kwa upande mwingine, kampuni ya Pwani Oil huchakata na kuziuzia supamaketi bidhaa zinazonunuliwa na wateja kwa kasi kama vile mafuta ya kupikia na sabuni.

Supamaketi ya Carrefour sasa imetakiwa kuzirejeshea kampuni hizo shilingi milioni 16.7 zilizotozwa kama kipunguo cha bei kutoka kwenye bili na shilingi laki 5 zilizotozwa kama usaidizi kwa soko.

Uchunguzi wa CAK pia umebaini kuwa kampuni zinazoiuzia supamaketi ya Carrefour bidhaa zinatakiwa kutoa bidhaa bila malipo na kulipa ada ya uorodheshaji kwa kila tawi la supamaketi hiyo linalofunguliwa na vilevile kupeleka wafanyakazi katika matawi hayo.

“Hatua hii ni sawa na kuhamishia gharama za supamaketi kwa wasambazaji bidhaa, kitu ambacho kimepigwa marufuku na Sheria ya Ushindani,” inasema CAK katika taarifa.

Hususan, kampuni ya Woodlands inatakiwa kupeana katoni moja kwa kila kitengo cha bidhaa zinazohifadhiwa na kulipa shilingi 50,000 kama masharti ya kuanza kusambaza bidhaa kwa matawi mapya ya supamaketi hiyo.

Kwa upande wake, kampuni ya Pwani Oil ilitakiwa kupeana katoni mbili bila malipo kwa kila kitengo cha bidhaa zinazohifadhiwa na kulipa shilingi laki 2 kama masharti ya kuanza kusambaza bidhaa kwa matawi mapya ya supamaketi hiyo.

Supamaketi ya Carrefour sasa imetakiwa kufanyia mabadiliko mikataba yote ya kampuni zinazoisambazia bidhaa na kuondoa vifungu vinavyowezesha utumiaji mbaya wa uwezo wake wa kufanya manunuzi.

Website |  + posts
Share This Article