Kamati ya Bunge la Taifa kuhusu ardhi imeingilia kati kusuluhisha mizozo ya ardhi inayohusisha kundi la kina mama la Wislon Mutumba eneo la Langata na kundi la kijamii la Kenanie katika eneo la Kenanie, kaunti ndogo ya Mavoko.
Kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Nyamira Joash Nyamok, ilikutana na makundi hayo kubainisha umiliki halisi wa ardhi nambari LR. 209/14582 na 12649 mtawalia.
Wanachama wa kamati hiyo walibainisha kuwa hakukuwa na makubaliano kupitia maandishi katika ya kundi la kina mama la Wilson Mutumba na shirika la Ireland kupitia mmiliki ambaye hakutajwa, anayedaiwa aliwasaidia kujenga nyumba za kukodi.
Vile vile, kamati hiyo ilidokeza kuwa kundi hilo la kina mama, lilitenga baadhi ya nyumba hizo kwa Huduma ya Taifa ya Polisi bila mintarafu kuelezea kuhusu kanuni za ushirikiano huo.
Kundi hilo la wanawake lilidai kwamba lilipewa cheti cha kukodi ardhi ambacho kilitolewa Disemba 18, 1990 na mwaka 1991, na kwamba lilisaidiwa kujenga nyumba za kukodi na shirika hilo la Ireland.
Ili kutatua kesi ya ardhi ya kundi la wanawake la Mutumba, kamati hiyo iliwahimiza kushirikisha wadau wengine walio na kesi sawia na hiyo mahakamani.
Katika kesi kuhusu kundi la kijamii la Kenanie, kundi hilo lilifahamisha kamati hiyo ya bunge kwamba, wanachama wake wameshindwa kuingia katika ardhi walioachiwa na mababu zao, wakidai kuwa ardhi hiyo ina sehemu ya kuabudu.
Ili kusitisha mzozo huo, kundi hilo la Kenanie, lilitaka kamati hiyo kuingilia kati kutatua suala hilo kubaini ikiwa ardhi hiyo inamilikiwa na shirika la huduma kwa wanyamapori KWS au jamii hiyo.
Wabunge hao waliagiza kundi hilo kusajili rasmi ardhi hiyo ili kuwezesha kamati hiyo kutatua suala hilo.