Bunge laidhinisha uteuzi wa Makamishna wapya wa IEBC

Tom Mathinji
1 Min Read
Vikao vya Bunge la Taifa.

Bunge la Taifa limeidhinisha uteuzi wa makamshina wote saba, waliopendekezwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wakiongea Jumatano alasiri wakati wa hoja ya kujadili ripoti ya kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Haki na Maswala ya Sheria(JLAC), wabunge wengi waliunga mkono ripoti  hiyo, wakisema idhini hiyo inaondoa kizingiti katika uundaji uliocheleweshwa wa tume hiyo muhimu.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wa, wabunge hao walisema kubuniwa kwa tume hiyo mpya kutaipa nchi hii muda wa kutosha, sio tu kujiandaa kwa uchaguzi mkuu ujao,lakini pia kuandaa chaguzi kadhaa ndogo zinazosubiriwa.

Kwa upande wake,mwasilishaji wa hoja hiyo ,ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya haki na sheria JLAC, George Murugara, alisema makamishna hao waliopendekezwa walipigwa msasa kikamilifu na kuthibitisha ufaafu wao kuhudumu katika tume hiyo.

Murugara hata hivyo aliwataka makamishna hao wapya waliopendekezwa kujenga imani ya umma, kwa kuandaa uchaguzi huru,haki na wa kuaminika.

Idhini hiyo sasa inampa Rais William Ruto fursa ya kuwateua rasmi makamishna hao, na kisha kuapishwa kuanza majukumu yao.

Website |  + posts
Share This Article