Bunge la Kitaifa lamuidhinisha Prof. Kindiki kuwa Naibu Rais

Martin Mwanje
2 Min Read

Bunge la Kitaifa limeidhinisha uteuzi wa Prof. Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais. 

Wabunge 236 wamepiga kura leo Ijumaa mchana kuidhinisha kuteuliwa kwa Prof. Kindiki kwenye wadhifa huo.

Wakati wa kikao hicho, hakuna mbunge aliyepinga au kukosa kupiga kura kuidhinisha uteuzi wa Prof. Kindiki ambaye hadi kuteuliwa kwake alikuwa Waziri wa Usalama wa Kitaifa.

Spika Moses Wetang’ula anasema sasa atatia saini Gazeti Rasmi la Serikali na kumtaarifu Rais kuwa Bunge la Kitaifa limeidhinisha uteuzi wa Prof. Kindiki kuwa Naibu Rais.

Kufuatia hatua ya bunge hilo, kinachosubiriwa ni kubaini ni lini Prof. Kindiki atakula kiapo cha kuhudumu kwenye wadhifa huo.

Ikizingatiwa kasi ya mchakato uliosababisha kutemwa kwa Gachagua, Prof. Kindiki huenda akaapishwa wakati wowote kuanzia sasa.

Rais William Ruto alimteua Prof. Kindiki kuwa Naibu wake baada ya Seneti kumtema Gachagua jana Alhamisi.

Hii ni baada ya bunge hilo kuridhia mashtaka 5 kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi ya Gachagua ikiwa ni pamoja na kueneza semi za chuki na ukabila.

Haya yanakuja huku timu ya wanasheria ya Gachagua ikifanya kila iwezalo kuzuia kuapishwa kwa mrithi wa mteja wao.

Naibu huyo wa Rais wa zamani anaendelea kupokea matibabu baada ya kukumbwa na maumivu makali ya kifua wakati wa vikao vya kusikiza mashtaka dhidi yake katika Bunge la Seneti.

Website |  + posts
Share This Article