Bunge la kitaifa linaandaa kikao maalum leo Jumatatu Mei 13, 2024 kujadili ripoti ya kamati ya muda ya wanachama 11 iliyopatiwa jukumu la kusikiliza madai dhidi ya waziri wa kilimo na ufugaji Mithika Linturi.
Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Naomi Waqo, mbunge wa kaunti ya Marsabit, ilikamilisha vikao vyake Ijumaa Mei 9, 2024 na kuanza kuandaa ripoti ambayo itawasilishwa bungeni leo.
Hoja ya kutaka kumwondoa afisini waziri Linturi iliwasilishwa na mbunge wa Bumula Jack Wamboka ambaye anamshtumu kwa kile anachokitaka kuwa kuidhinisha ununuzi na usambazaji wa mbolea gushi kwa wakulima.
Katika mawasilisho yake ya mwisho mbele ya kamati hiyo kupitia kwa wakili wake Muthomi Thiankolu, Linturi alikana kuhusika kwenye sakata hiyo akisema waziri kwa kawaida hahusiki moja kwa moja na manunuzi.
Badala yake alimwekea lawama mkurugenzi mkuu wa bodi ya nafaka na mazao NCPB.
Wakili Thiankolu alisema pia kwamba madai mengine dhidi ya Linturi kwenye kesi hiyo hayana uhusiano naye moja kwa moja.
Kwa upande wake Wamboka, alisisitiza kwamba waziri ndiye anafaa kuwajibikia makosa hayo akitaja athari walizokumbana nazo wakulima ambao walipokea mbolea gushi chini ya mpango wa kitaifa wa kugawa mbolea ya ruzuku.
Wakili wa Wamboka John Khaminwa, alimnyoshea Linturi kidole cha lawama kwa kukwaza mjadala akiongeza kusema kwamba mbolea gushi ilisambazwa na wa kuwajibishwa ni waziri husika.
Kamati hiyo kwa kauli moja ilikatalia mbali ombi la mshtakiwa la kuita katibu katika wizara ya kilimo Kipronoh Rono na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya KEL Chemicals kuipa ufahamu zaidi kuhusu sakata hiyo.
Tarehe 7 Mei 2024 kamati hiyo iliandaa kikao andalizi cha kusikiliza kesi, kesi ikaanza tarehe 8 ambapo Wamboka aliwasilisha ushahidi wake pamoja na mashahidi watano na tarehe 9 vikao vikafikia mwisho baada ya kumsikiliza waziri Linturi.
Leo wabunge watapata fursa ya kudurusu ripoti ya kamati hiyo, waijadili na mwisho waamue iwapo Linturi ataondolewa afisini au la.