Asilimia 65.11 ya Wakenya katika kiwango cha maeneo bunge waliunga mkono kubanduliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wakati wa zoezi la kukusanya maoni ya Wakenya lililoandaliwa mwishoni mwa wiki jana.
Katika ripoti yake juu ya zoezi hilo, bunge linasema jumla ya Wakenya 224,907 walitoa maoni yao.
Asilimia 33.80 walipinga hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Kulingana na ripoti hiyo, watu wengi waliounga mkono hoja ya kumbandua Gachagua walitoka ngome za kisiasa za Rais William Ruto, Spika wa bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga.
Kwa mfano, kulingana na ripoti hiyo, asilimia 99.26 ya wakazi wa eneo bunge la Baringo Kusini waliunga mkono kubanduliwa kwa Gachagua, Vihiga (89.40%), Rangwe (97.23%), na Mlima Elgon (99.16).
Maeneo ya kaskazini mwa nchi kama vile Mandera na Wajir yalishuhudia idadi kubwa ya Wakenya wakiunga mkono kubanduliwa madarakani kwa Naibu Rais.
Mathalan, asilimia 100 ya wakazi wote waliojitokeza katika eneo bunge la Balambala waliunga mkono hoja ya kutimuliwa kwa Gachagua.
Bunge kwa sasa linajadili hoja maalum iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi ya kutaka Gachagua aondolewa kwenye wadhifa huo.