Ubomozi wa nyumba umeanza katika eneo la Changamwe, kaunti ya Mombasa kwa lengo la kupisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu.
Wakazi wameonekana wakikimbia kuondoa vitu vyao kwenye nyumba zinazobomolewa wakati maafisa wengi wa polisi wakishika doria.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliangalia ubomozi wa nyumba hizo kwa macho makali wasiamini yaliyokuwa makazi yao wakati mmoja sasa yanageuka kuwa vifusi.
Ubomozi kama huo pia umeshuhudiwa katika eneo la Milimani katika kaunti ya Kakamega.
Utawala wa Rais William Ruto umesema unakusudia kujenga nyumba za gharama nafuu katika kaunti zote 47 nchini ili Wakenya wasiojiweza kiuchumi waweze kupata makazi mazuri ya kuishi.
Unasema ujenzi huo utatoa nafasi za ajira kwa maelfu ya vijana wasiokuwa na ajira humu nchini.
Akizungumza katika kaunti ya Meru jana Alhamisi, Rais Ruto alisema hadi kufikia sasa, ujenzi wa nyumba za bei nafuu umetoa fursa za ajira 130,000 kwa vijana nchini kufikia sasa.
Mahakama ya rufaa inatarajiwa kutoa uamuzi leo Ijumaa kuhusiana na ujenzi wa nyumba hizo leo Ijumaa.