Bodi yaagizwa kuchunguza madeni ya viwanda vya majani chai

Marion Bosire
2 Min Read
Katibu katika wizara ya Kilimo Dkt Kipronoh Ronoh.

Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Rono ameagiza uchunguzi wa mikopo yote iliyochukuliwa na viwanda vya majani chai vilivyo chini ya usimamizi wa mamlaka ya maendealeo ya majani chai nchini, KTDA.

Katika waraka alioandikia mkurugenzi mtendaji wa bodi ya majani chai nchini, Rono alisema hatua hiyo imechochewa na malalamishi ambayo yameibuka kuhusu tofauti katika malipo ya mikafaa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo imekuwa ikipokea malalamishi kutoka kwa wanaokuza majani chai kuhusu malipo ya kiwango cha chini ya mikafaa yaliyotolewa na viwanda vinavyosimamiwa na KTDA mwaka huu wa kifedha,” alisema Rono katika waraka huo.

Alisema malalamishi hayo yamesababisha uchunguzi wa kina wa majukumu ya kifedha na mitindo ya usimamizi ya viwanda vya majani chai nchini.

Rono alimwelekeza mkurugenzi wa bodi ya majani chai nchini kutekeleza uchunguzi wa mikopo ya viwanda, majibu yakitarajiwa kuonyesha kiwango jumla cha mikopo iliyochukuliwa na kila kiwanda na jinsi pesa hizo zilitumika.

Uchunguzi huo unastahili pia kufichua masharti ya mikopo hiyo na kiwango ambacho hakijalipwa kufikia sasa na kila kiwanda.

Kulingana na katibu Kipronoh majibu ya uchunguzi huo yataelekeza wizara ya kilimo katika kutathmini uendelevu wa kifedha wa kila kiwanda na kuunda sera za kukabili changamoto za sekta ndogo ya majani chai nchini.

Mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo ya majani chai anatarajiwa kuwasilisha majibu ya uchunguzi huo katika muda wa siku 14.

Website |  + posts
Share This Article