Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine amesema nyumba yake imezingirwa na maafisa wa usalama.
Wine alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe leo alipokuwa akirejea kutoka nje ya nchi na kusafirishwa moja kwa moja kwa ulinzi mkali hadi nyumbani kwake.
Katika ujumbe wake alioutuma kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) ulioambatana na picha za maafisa wa usalama, Bobi Wine amesema:
”Nyumba yetu bado imezungukwa na polisi na wanajeshi. Wamezuia watu wetu wengi kuingia kutusalimia. Hapo awali, walikuwa wakifyatua mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya. Niko chini ya kizuizi cha nyumbani. Utawala wa uhalifu katika hofu”
Awali Chama kikuu cha upinzani nchini Uganda nchini Uganda National Unity Platform (NUP) kilisema kiongozi wake Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine amekamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Entebbe alipokuwa akirejea kutoka nje ya nchi.
Chama cha (NUP) kilikuwa kikipanga kufanya mikutano na kuelezea kukamatwa kwake kama “mwoga”.
‘’Amechukuliwa akiwa bado kwenye ndege na kupelekwa katika maeneo yasiojulikana. Hadi muda huu hatujui yuko wapi,’’ Katibu Mkuu wa chama cha NUP David Lewis Rubongonya ameambia waandishi wa habari katika kituo cha ukaguzi wa kiusalama katika barabara kuu ya Entebbe Kampala ambapo alikuwa amezuiliwa kwenda uwanja wa ndege wa Entebbe kulingana na gazeti la Daily Monitor.
Kabla ya Kyagulanyi kurejea, polisi walikuwa wamesema msafara uliopangwa kutoka uwanja wa ndege haukuwa halali.
Hata hivyo, Daily Monitor imeweka ujumbe kwenye mtandao wa X na kumuonyesha mbunge Mathias Mpuuga akiwa na Bobi Wine nyumbani kwake Magere, wilaya ya Wakiso muda mfupi baada ya kukamatwa uwanja wa Entebbe.