Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken leo Ijumaa ameelezea matumaini ya kupatikana kwa suluhu ya kidiplomasia nchini Lebanon na kuzuia mgogoro mpana. Ameunga mkono juhudi za taifa hilo dhaifu kukabiliana na wanamgambo wa Hezbollah.
Blinken pia amesema Israel, ambayo imekuwa ikifanya mashambulizi yaliyosababisha vifo nchini Lebanon, “ina haki ya kujilinda” dhidi ya Hezbollah, lakini akaelezea hofu juu ya hali ya kibinadamu nchini Lebanon.
“Tunaendelea kufanya mawasiliano ya kina kuzuia mgogoro mpana katika eneo hilo,” Blinken aliwaambia wanahabari baada ya Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Asia Mashariki nchini Laos.
“Tuna shauku kubwa katika kujaribu kubuni mazingira ambapo watu wanaweza wakarejea kwenye makazi yao, wakahakikishiwa usalama wao, watoto wanaweza wakarejea shuleni,” alisema.
“Kwa hivyo Israel ina maslahi bayana na halali kabisa katika kufanya hilo. Watu wa Lebanon wanataka kitu sawia. Tunaamini kuwa njia bora ya kufika hapo ni kupitia uelewa wa kidiplomasia, ule ambao tumekuwa tukiufanyia kazi kwa muda, na ule ambao tunautilia maanani kwa sasa.”
Ameongeza kuwa Marekani itafanya kazi kuliunga mkono taifa dhaifu la Lebanon kujijenga upya baada ya kudhibitiwa kwa muda mrefu na Hezbollah.
“Ni wazi kwamba watu wa Lebanon wana maslhai — maslahi makubwa — katika taifa hilo kuchukua udhibiti na kuchukua wajibu kwa ajili ya nchi hiyo na mustakabali wake.”
Kulingana na Blinken, Marekani inaelezea mashaka yake moja kwa moja kwa Israel kuhusiana na hali ya kibinadamu katika eneo la Gaza.