Katibu katika idara ya uhamiaji na huduma kwa wananchi Julius Bitok, amesema wakenya wataweza kupata hati za kusafiria katika muda wa siku tatu baada ya kutuma maombi.
Akiongea leo Jumamosi katika eneo la Moiben, kaunti ya Uasin Gishu, Bitok alisema marekebisho yanayoendelea kufanywa yatawezesha hati hizo za usafiri kuwa tayari katika muda wa siku tatu kuanzia mwezi agosti mwaka huu.
Bitok alisema serikali inakaribia kukamilisha uwekaji wa mitambo ya kisasa ya kutayarisha hati hizo.Alisema kwa wakati huu huchukua muda wa wiki mbili kutayarisha hati hizo.
Katibu huyo alisema idara yake inasambaza huduma hizo ili kuhakikisha maeneo bunge yote yanazitoa.Bitok alifungua afisi ya usajii wa watu Moiben ili kupeleka huduma karibu na wananchi.