Mshindi wa nishani ya dhahabu ya mbio za mita mia nne wanariadha wanne kupokezana kijiti katika michezo ya Olimpiki mwaka 1972 Hezekiah Nyamau Munyoro, ameiaga dunia akiwa na umri wa miaka 82.
Nyamau aliyezaliwa katika kijiji cha Nyaguta,eneo bunge la Nyaribari Chache gatuzini Kisii vilevile alikuwa katika kikosi cha Kenya kilichoshinda nishani ya fedha katika mbio za mita mia nne wanariadha wanne kupokezana kijiti katika michezo ya Olimpiki mwaka 1968 nchini Mexico.
Kikosi hicho pia kilijumuisha wanariadha Daniel Rudisha,Naftali Bon na Charles Asati.
Vilevile Nyamau alikuwa bingwa wa michezo ya jumuiya ya madola mwaka 1970 na pia bingwa wa mbio za mita 400 kanda ya Afrika Mashariki na kati.
Akiwa na Robert Ouko, Julius Sang, na Charles Asati Nyamau aliishindia nishani ya dhahabu katika michezo hiyo ya Olimpiki mwaka 1972.
Nyamau alijiunga na kikosi cha majeshi mwaka 1963 na kustaafu mwaka 1997.
Chama cha riadha nchini kilimuomboleza mwanariadha huyo na kumtaja kuwa bingwa aliyewafungulia njia wanariadha wa mbio fupifupi wa kutoka humu nchini katika safu za kimataifa.