Bima ya SHIF: Wakenya wahaha kujisajili

Martin Mwanje
2 Min Read

Wakenya walikuwa na wakati mgumu kujisajili kwenye Bima mpya ya Afya ya Jamii, SHIF ambayo utekelezaji wake umepangiwa kuanza kesho Jumanne. 

Wizara ya Afya imetangaza makataa ya kujisahili kwenye bima hiyo kuwa leo Jumatatu.

Hata hivyo, Wakenya waliozungumza na KBC Digital Swahili walilalamika kuwa huku saa za kujisajili kwenye mfumo huo zikiyoyoma, iliguwa vigumu kujisajili kwani mfumo wa kujisajili ama ulikataa kufunguka au ulikwama muda mchache baada ya kufunguka.

Wizara ya Afya imewataka Wakenya kujisajili kupitia kwenye tovuti ya Mamlaka ya Afya ya Jamii ambayo ni https://sha.go.ke  au kupitia USSD Code *I47#.

“Nimejaribu lakini njia zote mbili za kujisajili zimekataa. Nitasubiri wizara irefushe muda wa kujisajili. Sina budi,” alisema raia mmoja aliyezungumza na KBC Digital Swahili ingawa hakutaka kutambuliwa.

“Nadhani mfumo unakataa kwa sababu watu wengi wanakimbilia kujisajili kabla ya kumalizika kwa makataa.”

Bungeni, alipofika mbele ya Kamati ya Afya inayoongozwa na mbunge wa Endebes Dkt. Robert Pukose, Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa alikuwa na wakati mgumu kueleza namna Wakenya wenye kipato cha chini watakavyokatwa pesa chini ya bima hiyo mpya itakayochukua mahali pa ile ya NHIF.

Hata hivyo, licha ya mashaka yaliyoibuliwa na wabunge, Dkt. Barasa amewahakikishia Wakenya kuwa serikali iko tayari kutekeleza bima mpya ya afya ya jamii ya SHIF.

Kwa mujibu wa bima hiyo, Wakenya wanaopata mshahara wa jumla ya shilingi 20,000 watatozwa shilingi 550 kugharimia bima hiyo, 50,000 shilingi 1,375, 100,000 shilingi 2,750, 200,000 shilingi 5,500, 500,000 shilingi 13,750 huku Wakenya wanaopata mshahara wa shilingi milioni moja wakitozwa shilingi 27,500.

 

Share This Article