Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa zamani wa Marekani ambaye pia ni mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump, walishiriki mdahalo wa CNN wa wagombea urais wa uchaguzi wa mwaka 2024, huko Atlanta, Georgia, Juni 27, 2024.
Wawili hao walirushiana cheche za maneno, huku kila mmoja akilenga kutafuta uungwaji mkono wa wapiga kura, kabla ya uchaguzi mkuu baadaye mwezi Novemba mwaka huu.
Trump alimlaumu Biden kuhusu uchumi, rekodi yake ya sera za kigeni na uhamiaji, huku Biden akilenga hukumu za hivimajuzi za uhalifu dhidi ya Trump na kile anachosema ni tishio kwa demokrasia.
Hii ni mara ya pili kwa Biden na Trump kukutana katika mdahalo wa kuwania urais,baada ya trump kushindwa katika kinyang’anyiro hicho mwaka 2020.
Mdahalo huu ulitoa fursa kwa wagombea hao wawili kujaribu kutengeneza tena maelezo ya kisiasa na kuwashawishi wapiga kura waliokuwa hawana uamuzi wampe nani kura zao.
Baada ya mdahalo huo, Biden alisimama katika hoteli moja iliyokuwa karibu ambapo wafuasi wake walikuwa wakifuatilia.