Shirika la kutafisiri Biblia la Bible Translation & Literacy (BTL) limezindua Biblia iliyotafisiriwa kwa lugha ya Kichonyi.
Uzinduzi huo ulifanyika katika eneo la Chonyi, eneo bunge la Kilifi Kusini.
Tafsiri ya Biblia hiyo ilianza mnamo mwaka wa 2013 na utafiti wa isimu lugha ya Kichonyi na kisha uendelezaji wa kozi ya tahajia kwa gharama ya shilingi milioni 40.
Kichonyi ni moja ya lugha ya tisa zinazozungumzwa na Wamijikenda, na wazungumzaji wake wanapatikana eneo bunge la Kilifi Kusini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Kitaifa wa BTL Rev.Peter Munguti aliwalimbikizia sifa wana isimu, wabobezi, na jamii ya eneo hilo kwa kujitolea kufanikisha mradi huo.
Rev. Munguti aliongeza kuwa kutafisiriwa kwa Biblia ni muhimu kwa Wachonyi kwa sababu hatua hiyo itasaidia kukabiliana na tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile uchawi na kuchochea maendeleo ya jamii hiyo.
‘‘Tumesikia simulizi nyingi za wazee kuuawa katika eneo hili. Tunatazamia kwamba baada ya kusoma neno la Mungu katika lugha yao, jamii hiyo itakumbatia usasa.”
Mchungaji huyo aliihakikishia jamii hiyo kuwa Biblia italinda lugha ya Kichonyi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
‘‘Tafsiri hizi zinasaidia vizazi vijavyo kupata lugha yao ikiwa salama na kudumisha tamaduni muhimu,’’ aliongeza Rev. Munguti.
Ufasiri wa Biblia ni sanaa ya kutafsiri neno la Mungu katika lugha zingine kutoka lugha halisi.
Mchungaji huyo alisema ufasiri unaofanywa na BTL haukinzani na Biblia halisi iliyoandikwa katika lugha za Kigiriki na kiebrania.
‘‘Mamlaka yetu ni kueneza neno la Mungu bila kulibadilisha. Kwa hivyo, toleo hili linawiana na toleo la kwanza lililoandikwa katika lugha za Kigiriki na Kiebrania.”
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Mradi huo Askofu Reuben Mungunya Lewa alisema Biblia hiyo itatia makali mahubiri yao na kueneza upendo katika jamii hiyo.
“Jamii ya Chonyi inawapoteza wazee siku baada ya siku kwa sababu ya uchawi, na kwa Biblia hii, tuko tayari kueneza upendo wa Mwenyezi Mungu kwa kila mtu,” alisema Askofu Lewa.
Mwenyekiti wa Bodi ya BTL Kendi Ogamba aliwahakikishia wakazi kwamba shirika hilo litaimarisha kazi yake ili kuhitimisha ufasiri wa Biblia.
‘‘Kile ambacho tumefanya leo ni mwanzo wa ufasiri wa Agano la Kale. Hatutakoma hadi Wachonyi wapate tafsiri ya Agano la Kale na Agano Jipya.”