Mwanamuziki wa Marekani Beyonce anaendelea kutafuta usajili wa jina la binti yake Blue Ivy kama nembo ya kibiashara.
Mawakili wake wanaendelea kuvutana na afisi ya usajili wa nembo nchini Marekani, miaka 12 baada ya kunyimwa haki hiyo ya kusajili nembo.
Waliwasilisha ombi jingine kwa afisi hiyo ya usajili wiki iliyopita kupinga uamuzi wa mapema mwaka huu uliodai kwamba watumiaji wa bidhaa wangekanganyika kwa sababu kuna duka la nguo Blue Ivy.
Duka hilo ambalo halina matawi mengine liko Wisconsin, na limekuwa likitumia jina hilo tangu wakati Blue Ivy Carter hakuwa amezaliwa.
Wanataka uamuzi huo ubatilishwe kwa sababu wanaamini hakuna mtu anaweza kukanganyika kuhusu Blue Ivy Carter kwa sababu yeye ndiye mtoto maarufu zaidi ulimwenguni.
Mwaka 2012, wiki chache baada ya Blue Ivy kuzaliwa, mawakili wa kampuni ya BGK Trademark Holdings LLC waliwasilisha maombi ya kusajili jina lake kama nembo.
Wengi walishangazwa na hatua hiyo lakini Jay-Z alielezea kwamba walitaka tu kutunza jina la mwanao lisitumiwe ovyo ovyo na watu wengine.
Mchakato huo umekumbwa na kesi kadhaa mahakamani zilizowasilishwa na Veronica Morales, ambaye anamiliki kampuni ya kuandaa hafla na ya mitindo iitwayo “Blue Ivy” na ambayo tayari alikuwa amesajili kama nembo.
Hata hivyo mahakama ilikataa maombi yake ikisema hakuna mkanganyiko wa namna yoyote kwani nembo yake ni tofauti na jina la mtoto huyo ikitizamiwa shughuli za nembo hiyo.
Uamuzi huo ni kama ulifungua mwanya wa kupata usajili wa nembo ya jina “Blue Ivy Carter” lakini mawakili wa Beyonce wakakosa kufuatilia na mahakama ikachukulia kwamba kesi hiyo imetelekezwa.
Novemba 2023, waliwasilisha ombi la kusajili nembo hiyo lakini bado ikagonga mwamba. Mwezi aprili mwaka huu, msajili wa nembo aliamua kwamba jina hilo lilikuwa linafanana sana na nembo ambayo tayari imesajiliwa.