Bendera za mahakama kupeperushwa nusu mlingoti

Marion Bosire
2 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome

Jaji mkuu Martha Koome ameelekeza kwamba bendera zote za idara ya mahakama katika vituo vya idara hiyo kote nchini zipeperushwe nusu mlingoti kama njia ya kutoa heshima kwa hakimu Monica Kivuti.

Koome alitoa maelekezo hayo kwenye taarifa rasmi ya kutangaza kifo cha hakimu Kivuti aliyeaga dunia akipokea matibabu kutokana na majeraha ya risasi.

Alisema bendera hizo zitapeperushwa nusu mlingoti hadi pale atakapozikwa hakimu Kivuti.

Koome ambaye alizuru familia ya marehemu Kivuti jana Jumamosi, alielezea kwenye taarifa hiyo kwamba alipata fursa ya kumzuru Kivuti hospitalini Ijumaa Juni, 14, 2024 saa sita mchana akiwa na jaji mkuu mstaafu David Maraga na maafisa wengine wa idara ya mahakama.

Kulingana naye, ripoti waliyopatiwa na madaktari wakati huo kuhusu matibabu ya Kivuti ilikuwa ya kuridhisha kwani waliarifiwa kwamba alikuwa anapata nafuu ila saa chache baadaye wakapokea ripoti kwamba amefariki.

Jumanne 18, Juni, 2024 imetangazwa kuwa siku ya wahusika wote wa idara ya mahakama kusimama na familia ya hakimu Kivuti huku wakimkumbuka na kutoa heshima kwake.

Kutokana na hilo, hakuna mahakama itaendeleza kazi za kawaida siku hiyo na badala yake vikao vya kumuenzi Kivuti vitaandaliwa katika vituo vyote vya mahakama kote nchini.

Kituo cha mahakama cha Makadara ambako mkasa ulitokea kitafungwa hadi Jumatatu Juni 24, ili kutoa nafasi kwa kubomolewa kwa maeneo ya muda ya kusikilizia kesi na kuimarishwa kwa usalama.

Hakimu Kivuti alipigwa risasi na afisa wa polisi aliyekuwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi ya mke wake, punde baada ya kutoa uamuzi ambao haukumridhisha.

Afisa huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi waliokuwa mahakamani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *