Belarus kufanya uchaguzi wa urais Januari 26

Martin Mwanje
1 Min Read
Alexander Lukashenko - Rais wa Belarus

Tume ya uchaguzi nchini Belarus leo Jumatano imetangaza kuwa nchi hiyo itafanya uchaguzi wa urais Januari 26 mwakani. 

Belarus, mshirika mkuu wa Urusi, imetawaliwa na kiongozi wa kidikteta Rais Alexander Lukashenko tangu mwaka 1994.

Lukashenko ameondoa aina zote za upinzani na mnamo mwezi Februari mwaka 2022, aliruhusu jeshi la Urusi kuanzisha operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Ukraine kutoka eneo la Belarus.

Kwenye taarifa katika mitandao ya kijamii, tume ya uchaguzi imesema bunge limeidhinisha tarahe ya kufanywa kwa uchaguzi huo.

Wakosoaji wanamshtumu Lukashenko, ambaye anatarajiwa kugombea tena wadhifa huo, kwa kuongoza nchi hiyo inayoendelea kuwa ya kidikteta, kuminya haki za kibinadamu na kuwafunga jela wapinzani wake wa kisiasa.

Uchaguzi wa mwisho wa urais mwaka 2020 ulikumbwa na udanganyifu na kusababisha maandamano makubwa yaliyodumu wiki kadhaa.

Mpinzani wa Lukashenko wakati wa uchaguzi huo wa mwaka 2020, Svetlana Tikhanovskaya, alidai kuibuka mshindi lakini pia alilazimishwa kuondoka nchini humo.

Share This Article