Baraza la Vyombo vya Habari nchini, MCK limeshutumu mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya wanahabari wakati wa maandamano ya vijana wa Gen Z katika maeneo mbalimbali humu nchini.
Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo David Omwoyo alisema visa 24 vya ukatili wa polisi dhidi nya wanahabari wakiwa kazini viliripotiwa.
Kulingana naye, taasisi husika zimekusanya ushahidi ili kuwezesha kushtakiwa kwa maafisa wa polisi waliotekeleza ukatili huo.
Omwoyo anaitaka Mamlaka ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi, IPOA, Afisi ya Mkurugezi wa Mashtaka ya Umma, ODPP na Inspekta Jenerali wa Polisi kuharakisha uchunguzi na kuwachukulia hatua wahusika.
Akiongea mjini Naivasha wakati wa mkutano wa wadau wa vyombo vya habari, Omwoyo alisema ipo haja ya kuimarisha uhusiano kati ya serikali na vyombo vya habari katika harakati za kuwahakikishia wanahabari usalama wao.
Paul Ilado ambaye ni mwanachama wa Chama cha Wahariri, KEG ameshauri wanahabari kuripoti mashambulizi yoyote yanayotekelezwa na polisi ili washtakiwe.
Mwenyekiti wa Tume ya Kushughulikia Malalamishi ya Vyombo vya Habari Demas Kiprono alisema malalamishi manane yamepokelewa kuhusiana na ukiukaji wa uhuru wa vyombo vya habari na wanapania kuyashughulikia kupitia mashauriano.
Alisisitiza kwamba uhuru wa vyombo vya habari umehakikishwa na kifungu nambari 34 cha katiba ya Kenya na hivyo uanahabari ni muhimu sana kwa demokrasia.