Baraza la mawaziri limewaagiza wananchi wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na hatari, kuhamia maeneo salama katika muda wa saa 48.
Kulingana na baraza hilo la mawaziri, maeneo hayo ni pamoja na yale yaliyo karibu na mabwawa,hifadhi za maji katika ardhi ya umma na zile za kibinafsi, maeneo yaliyo na hatari ya maporomoko ya ardhi na karibu ni mito kote nchini.
Katika mkutano wake leo Jumanne asubuhi ulioongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, baraza hilo lilisema wale ambao wataathiriwa na agizo hilo, watajulishwa kufikia May 1, 2024.
“Serikali imeweka mikakati ya kupiga jeki zoezi hilo pamoja na makazi ya muda kwa wale watakaoathiriwa na agizo hilo na hawana makazi mbadala,” ilisema taarifa kutoka Ikulu ya Nairobi.
Wakati huo huo, serikali imesema imetambua maeneo ya umma kote nchini ambako watu watapewa makazi ya muda, pamoja na vyakula na mahitaji mengine ya msingi.
Hata hivyo wale ambao watakaidi agizo hilo la serikali, watahamishwa kwa nguvu ili kulinda usalama wao.
Maafisa wa serikali ya kitaifa pia wameagizwa kushirikiana na maafisa wa serikali za kaunti, mashirika ya kibinadamu na wadau wengine, kuhakikisha shughuli ya kuwahamisha watu na kuwapa makazi inatekelezwa kwa wakati na kwa njia ya kibinadamu.