Baraza la Mawaziri laidhinisha mpango wa kukabiliana na pombe haramu

Marion Bosire
2 Min Read

Baraza la Mawaziri limeidhinisha hatua zilizochukuliwa na serikali katika vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya humu nchini.

Hatua hizo zilizotangazwa na Wizara ya Usalama wa Kitaifa ni pamoja na kufutiliwa mbali kwa leseni zote 52 za watengenezaji wa pombe za kiwango cha pili kwa siku 21 na kufutiliwa mbali kwa leseni zote za baa zilizotolewa na serikali za kaunti.

Nyingine ni pamoja na misako ya kila mara kote nchini ya kupambana na uuzaji, usafirishaji, usambazaji na unywaji wa pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya.

Baraza la Mawaziri limepitisha kwamba afisa yeyote wa serikali ambaye atapinga hatua hizo atakuwa anakiuka sura ya sita ya katiba na sheria za mkinzano wa maslahi.

Maafisa hao ni pamoja na polisi, wawakilishi wa serikali kuu mashinani, maafisa wa kukusanya ushuru, wa kukadiria ubora wa bidhaa, wa afya ya umma na waendeshaji wa mashtaka kati ya wengine.

Baraza hilo lilifahamishwa kwamba tangu Wizara ya Usalama wa Kitaifa ianzishe utekelezaji wa hatua hizo, biashara za pombe 2,393, maduka ya dawa 359 na maduka 452 ya bidhaa za shambani na mifugo yamefungwa.

Katika kikao kilichoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi leo, Baraza la Mawaziri lilifahamishwa pia kwamba maeneo 5,835 ya biashara ya pombe yamevamiwa ambapo lita 289,390 za pombe haramu na nyingine 13,198 za pombe haramu zimenaswa.

Share This Article