Baraza la Vyama vya Soka katika eneo la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na Baraza la Vyama vya Soka katika eneo la Kusini mwa Afrika (COSAFA) yametangaza kushirikiana kuunga mkono wagombea wao katika uchaguzi ujao wa Baraza la FIFA.
Kinara wa COSAFA Said Ali Said Athouman na kinara wa CECAFA Wallace Karia walitoa taarifa ya pamoja kuthibitisha dhamira yao ya kuwaunga mkono wagombea hao wawili kutoka maeneo yao.
COSAFA, inayowakilisha mashirikisho 14 wanachama wa CAF, imemteua Andrew Kamanga, kinara wa Chama cha Soka cha Zambia, ilihali CECAFA, inayoundwa na mashirikisho 11 wanachama wa CAF, imemteua Souleiman Waberi, kinara wa Shirikisho la Soka la Djibouti.
Kamanga na Waberi wote wameidhinishwa kuwania nafasi hizo na kamati ya FIFA inayosimamia uchaguzi huo.
Ushirikiano kati ya COSAFA na CECAFA unaangazia mshikamano wa kikanda kwani mashirika yote mawili yananuia kupata nafasi kwenye Baraza la FIFA, huku CAF ikiwa na nafasi tano katika baraza hilo la FIFA.