Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen leo Jumamosi alifungua rasmi barabara ya kuondoka kwa ile ya Expressway, kwenye mzunguko wa barabara ya Haile Selassie inayoingia katikati ya jiji la Nairobi.
Barabara hiyo iko katika eneo la Greenpark na imekuwa ikijengwa kwa muda wa miezi mitano.
Ufunguzi wa barabara hiyo unatarajiwa kupunguza msongamano na kuboresha usafiri kuelekea katikati ya jiji, maeneo ya Upper Hill na barabara ya Ngong.
Waziri Murkomen alitoa wito kwa wakenya wadhamini maendeleo ya miundomsingi inayotekelezwa na serikali, ambayo inanuiwa kupata kwa urahisi huduma za serikali katikati mwa jiji.
“Umuhimu wa barabara ya Expressway ulipuuzwa kwa sababu hakuwa na barabara ya kuondoka expressway katika eneo la katikati mwa Jiji la Nairobi, hasaa katika barabara ya Harambee ambako kuna afisi za serikali, zikiwemo afisi ya Rais, ile ya naibu rais, bunge na idara ya Mahakama. Serikali haikuwa ikihudumiwa na barabara hiyo,” alisema waziri Murkomen.
Kulingana na waziri Murkomen, mradi wa barabara ya Expressway, imetoa nafasi 500 za ajira za kudumu.
Murkomen alidokeza kuwa serikali inalenga kuazisha miradi zaidi ya ujenzi wa barabara kama ile ya kuweka safu mbili barabara ya Rironi-Mau Summit, ile ya Nairobi-Mombasa barabara ya ya Athi River-Namanga, Kisumu-Isibania na barabara ya Kiambu.