Polisi mjini Malindi, kaunti ya Kilifi wanamsaka mshukiwa wa ulanguzi wa mihadarati aliyekwepa mtego wa polisi na kuacha nyuma bangi yenye thamani ya shilingi milioni 2.5.
Morris Ware alisakwa na polisi baada ya raia kuwapasha habari kuwa alimiliki bangi hiyo.
Ni hatua iliyofanya wapelelezi kutoka kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya katika kituo cha polisi cha Malindi kuvamia duka lake kijijini Midodoni.
“Hata hivyo, mshukiwa alikimbia baada ya kuwaona maafisa na kuacha duka lake likiwa halina mtu,” ilisema Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI katika taarifa.
“Katika duka hilo, maafisa walipata kilo 86 za bangi zilizokuwa zimewekwa kwenye magunia manne ambayo hayakufunikwa chochote na ambayo thamani yake ni shilingi milioni 2.5.”
Bangi hiyo ilipelekwa katika kituo cha polisi cha Malindi huku msako dhidi ya mshukiwa ukiendelea.