‘Baba Yao’ kusalia jela akisubiri uamuzi wa mahakama

Martin Mwanje
1 Min Read
Ferdinand Waititu - Gavana wa zamani wa Kiambu

Gavana wa zamani wa kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu almaarufu “Baba Yao” alipata pigo leo Jumatano baada ya Mahakama Kuu kuamuru kuwa asalie gerezani hadi Aprili 23.

Waititu, kwa mara ya pili, alikuwa akijaribu kutaka aachiliwe kwa dhamana hadi rufaa aliyowasilisha kupinga  kifungo chake cha miaka 12 jela isikilizwe na kuamuliwa.

Jaribio sawia liliambulia patupu Machi 3 mwaka huu baada ya Jaji Lucy Njuguna kukatalia mbali ombi hilo. 

Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ilimhukumu Waititu kifungo cha miaka 12 jela baada ya kupatikana na hatia katika sakata ya utoaji zabuni ya shilingi milioni 588.

Waititu, ambaye alipatikana na hatia Februari 13, alihukumiwa kwa kutoa kandarasi ya kukarabati barabara kaunti ya Kiambu katika mwaka wa kifedha wa 2017-2018  bila kufuata taratibu za kisheria.

Mahakama hiyo pia ilimzuia Waititu kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa muda wa miaka 10.

Washtakiwa wenzake, akiwemo mkewe  Susan Wangari, pia walihukumiwa, huku Wangari akitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Testimony Enterprises Charles Chege, alitozwa faini ya shilingi milioni 295, huku mhandisi wa barabara Lucas Wahinya akitozwa faini ya shilingi milioni 21.

Website |  + posts
Share This Article