Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, wamemkamata baba na mwana wake wa kiume, wanaodaiwa kuhusika na wizi wa fedha katika soko la Gikomba.
Peter Mwendwa Musyoka mwenye umri wa miaka 49 na mwaka wake Dennis Musyoka mwenye umri wa miaka 29, walikamatwa kutoka maficho yao katika mtaa wa Komarock Jijini Nairobi baada ya kuhusishwa na wizi wa shilingi 236,000 kupitia mfumo wa malipo wa M-pesa mnamo Septemba 2, 2025.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema baada ya kupekua nyumba ya washukiwa hao, maafisa hao walipata vitambulisho vya taifa, namba za paybill kutoka Safaricom, Telcom, Airtel, vipakatalishi na simu za rununu zinazoaminika kutumiwa katika ulaghai huo.
Maafisa hao wanaamini kuwa baba huyo ndiye anayemfunza mwana wake kuendesha biashara hiyo haramu ya kuwaibia waibia wahudumu wa M-Pesa.
Kwa sasa wawili hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani, huku polisi wakiendelea kuwasaka washukiwa wengine.