Baadhi ya wawakilishi wadi katika kaunti ya Nyandarua wamejitenga na mjadala unaotarajiwa wa kumbandua mamlakani Gavana Moses Kiarie maarufu kama Badilisha.
Wakizungumza katika bunge la kaunti hiyo ya Nyandarua, wawakilishi wadi 21 walisema hawataunga mkono mjadala huo uliowasilishwa na mwakilishi wa wadi ya Mirangine Samuel Mathu.
Wakiongozwa na kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo Mwangi Nyaga, wawakilishi wadi hao walisema hatua hiyo imejiri wakati usiofaa.
Nyaga alisema kwa sasa wanaangazia maendeleo na wala sio sarakasi za kisiasa.
“Tunasema wazi kwa watu wa Nyandarua kwamba sio wakati wa siasa bali ni wakati wa maendeleo. Hata hatutambui mjadala huo.” alisema.
Mwakilishi wadi huyo alidai kwamba karibu wawakilishi wadi wote 41 hawaungi mkono mjadala huo.
“Tunaunga mkono kikamilifu usimamizi wa sasa. Wakati wa siasa uliisha tulipoingia madarakani.” Alisema Nyaga.
Kiongozi wa wachache katika bunge la kaunti ya Nyandarua Mwangi Gichuki naye alitetea serikali ya kaunti akisema imetekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi.
“Tumeona barabara zikijengwa, maji yakiwekwa na uimarishaji wa kilimo.” alisema Gichuki akishangaa ni kwa nini wanakumbushwa ya kale.
Alisema iwapo mjadala huo utafuata mchakato unaofaa basi utawakuta bungeni.