Huku mitihani ya darasa la nane na ile ya gredi ya sita ikianza leo Jumatatu, baadhi ya wanafunzi wa darasa la nane na wale wa gredi ya sita katika kaunti ndogo ya Narok kaskazini, watakosa kufanya mitihani hiyo baada ya serikali kutangaza kuwa shule zao si halali.
Shule za msingi za Sasimwani na Enesonkoyo ambazo ni vituo vya kufanya mtihani wa kitaifa kwa wanafunzi wa darasa la nane, ziko katika msitu wa Maasai Mau, ardhi ambayo inalengwa katika zoezi la kuwahamisha waliovamia msitu huo.
Wazazi wa wanafunzi hao wakiongozwa na Christopher Kuyioni, mchungaji Joseph Dikirr na Oloodo Kuyioni, walilalamika kuwa watoto wao wametatitiza kiwamazo kutokana na kuhamishwa kutoka eneo hilo baada ya nyumba zao kubomolewa.
“Zaidi ya maafisa 100 kutoka maafisa wa kulinda misitu KFS,wale wa huduma kwa wanyamapori KWS na maafisa wa polisi, walibomoa nyumba zetu na waliharibu mimea yetu,”alisema Kuyioni.
Akizungumza kando ya vifusi vya nyumba yake iliyobomolewa, Kuyioni alisema hana pa kwenda kwa kuwa babake ambaye ana umri wa miaka 100 alizaliwa katika eneo hilo.
Kwa upande wake, mchungaji Joseph Dikirr alitoa wito kwa Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu kuingilia kati kwa kuwa hawana pahali kulala.