Baadhi ya madaktari wanagenzi kuanza kazi Agosti

Marion Bosire
2 Min Read

Wizara ya Afya nchini imetangaza kwamba baadhi ya madaktari wanagenzi wataanza kazi Agosti Mosi, 2024.

Hatua hii inafuatia kutiwa saini kwa ongezo la makubaliano ya kurejea kazini kati ya wizara hiyo na madaktari yaliyotiwa saini kwa mara ya kwanza Mei 8, 2024.

Ongezo lililotiwa saini leo na katibu wa afya ya umma Mary Muthoni na viongozi wa chama cha madaktari KMPDU wakiongozwa na Daktari Davji Atellah linafutilia mbali barua za fursa kwa madaktari wanagenzi zilizotolewa Machi 18, 2024.

Stakabadhi hiyo ambayo imetiwa saini leo huku mazungumzo yakiendelea ya kutatua matakwa yote yaliyoibuliwa na madaktari inakubalia kutumwa nyanjani mara moja kwa madaktari wanagenzi 1210.

Kuhusu malipo ya wanagenzi hao, Muthoni alisema kwamba suala hilo bado linajadiliwa na litatatuliwa kulingana na uamuzi wa mwisho wa mahakama ya wafanyakazi mjini Eldoret.

Malimbikizi yote ya kabla ya uamuzi huo wa mahakama katibu huyo alisema yatalipwa kikamilifu katika muda wa siku tisini kuanzia siku ya uamuzi huo wa mahakama.

Huku akishukuru wanachama wa KMPDU kwa kujitolea kwao kwa mpango mzima wa majadiliano, katibu Muthoni alisema kama wizara wanatambua masuala yote yanayoendelea mahakamani kuhusu wahudumu wa afya.

Aliongeza pia kwamba wanatambua kubuniwa kwa kikosi kazi cha Rais cha kushughulikia masuala ya nguvukazi katika sekta ya afya Julai 5, 2024 ambapo wanachama wa KMPDU pia wamejumuishwa.

Madaktari wanagenzi wamekuwa wakiandamana nje ya afisi za wizara ya Afya jijini Nairobi kulalamikia kutotumwa nyanjani hata baada ya kukamilisha masomo yao.

Lalama zao zilikuwa sehemu ya zile za chama cha KMPDU ambacho kiliandaa mgomo wa madaktari, mgomo ambao ulitamatishwa bila mwafaka kamili kuhusu mustakabali wa madaktari wanagenzi ndiposa wakaanzisha maandamano yao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *