Muungano wa Azimio umelalamikia kile unachodai ni hatua ya maafisa wa polisi kuwakamata watu wanaoonekana kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Muungano unasema vijana waliotekwa nyara ni wale wanaoonekana kuwa na ushawishi katika mitandao ya kijamii.
Kulingana nao, wa hivi punde kukamatwa ni Gabriel Oguda ambaye ni mchambuzi wa masuala ya sera katika ofisi ya kiongozi wa walio wachache Opiyo Wandayi katika bunge la taifa.
Opiyo ameliambia bunge kuwa Oguda alitekwa nyara na watu wasiojulikana saa nane usiku na kuwalaumu polisi kwa utekaji huo.
Kulingana na Azimio, vijana wengine waliokamatwa kufikia sasa ni John Frank Ngemi, Shadrack Kiprono, Drey Mwangi, Ernest Nyerere, Kevin Monare, Harieth Nyongesa na Zadock Machiavelli.
Akiwahutubia wanahabari katika majengo ya bunge leo Jumanne, Seneta wa kaunti ya Kilifi Sewart Madzayo amewatuhumu polisi kwa utekaji nyara huo na kutoa wito wa kuachiliwa kwa vijana hao mara moja.
Shirika la kutetea haki za bindamau la Amnesty International limenukuliwa likisema hadi kufikia sasa, vijana 12 wametekwa nyara na kile kinachoaminika kuwa maafisa wa usalama.