Muungano wa Azimio umesisitiza kuwa maandamano yaliyoratibiwa kufanyika juma hili yataendelea kama ilivyopangwa.
Muungano wa Azimio umeitisha maandamano siku za Jumatano, Ahamisi na Ijumaa kulalamikia kupanda kwa gharama ya maisha na kupitishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023.
“Maandamano ya amani yaliyopangwa kufanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa juma hili yataendelea kama ilivyotangazwa awali na viongozi wetu,” alisema kiongozi wa wachache katika bunge la Taifa Opiyo Wandayi wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu.
“Maandamano haya yataendelea kwa mujibu wa kufungu nambari 37 cha katiba yetu kinachoruhusu kufanyika kwa maandamano ya amani. Hakuna mtu yeyote au taasisi iliyo na mamlaka ya kusitisha kutekelezwa kwa kifungu hicho.”
Hata hivyo, utawala wa Kenya Kwanza ukiongoza na Rais William Ruto umetangaza kuwa hakuna maandamano yatakayoruhusiwa kufanyika nchini wiki hii, ukitaja maafa na uharibifu wa mali ulioshuhudiwa wakati wa maandamano ya Azimio Jumatano juma lililopita.
“Mimi nataka niwaambie, maandamano haiwezi tena kufanyika katika taifa hili letu la Kenya. Hiyo wanasema Wednesday, hiyo wanasema sijui lini, hiyo maandamano haiwezekani. Haiwezekani,” alionya Rais Ruto wiki jana alipowahutubia raia wakati wa uzinduzi wa barabara ya Njabini kuelekea Naivasha katika kaunti ya Nakuru.