Watahiniwa 965,501 wa mtihani wa kitaifa KCSE, leo Jumatatu wameanza awamu ya pili ya mtihani huo ambao ni mtihani wa kuandika.
Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt.. Raymond Omollo, alisambaza mtihani huo katika kaunti ya Kiambu, Jumatatu asubuhi.
Mtihani huo ulianza saa mbili kamili asubuhi kwa somo la kiingereza na baadaye somo la kemia wakati wa alasiri.
Baraza la mitihani hapa nchini,KNEC , limeweka mikakati mipya ya kudhibiti udanganyifu kwenye mtihani huo.
katika kudumisha usalama wa mtihani huo, afisa mkuu mtendaji wa KNEC David Njeng’ere alisema kontena za mitihani zitafunguliwa saa moja kamili kote nchini, ili kutoa nafasi ya usambazaji karatasi za mtihani kwa wakati.
Maafisa wote pia katika vituo vya mitihani hawatakubalika kuwa na simu za rununu, kwani zinafaa kufungiwa na funguo ziwe na msimamizi wa mitihani katika kituo husika.
Wasimamizi wa vituo vya mitihani ambao kwa kawaida ni walimu wakuu wamejukumika kuhakikisha ni watu walioidhinisha wanaohusika na mitihani.
Mtihani huo ambao utaendelea hadi tarehe 22 mwezi Novemba unafanywa katika vituo 10,755 kote nchini.