Aliyekuwa kiongozi wa Myanmar Aung San Suu Kyi ambaye aliwahi kushinda tuzo ya Nobel amesamehewa makosa matano kati ya yote 19 na jeshi la nchi hiyo.
Alipatwa na hatia mahakamani kwa makosa hayo na kuhukumiwa kifungo cha miaka 33 gerezani. Msamaha huo uliotangazwa leo Jumanne ni sehemu ya msamaha uliotolewa kwa wafungwa wapatao elfu 7 kama njia ya kusherehekea kwaresma ya Wabudha.
Aung San Suu Kyi ambaye anasemekana kuhamishwa kutoka jela wiki jana na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani jijini Naypyidaw, amekuwa kizuizini tangu jeshi lilipopindua serikali yake mwanzoni mwa mwaka 2021.
Kwa sasa amekata rufaa kwa makosa aliyoshtakiwa kama vile uchochezi, udanganyifu katika uchaguzi na ufisadi, makosa ambayo alikana mbele ya mahakama.
Kiongozi huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 78 bado anakabiliwa na mashtaka 14 na hivyo ataendelea kuzuiliwa nyumbani.
Aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Win Myint naye alipunguziwa hukumu chini ya msamaha huo wa kwaresma.
Aung San Suu Kyi ni binti ya shujaa wa uhuru wa Myanmar Aung San na alifungwa kifungo cha nyumbani mara ya kwanza mwaka 1989 baada ya maandamano makubwa dhidi ya utawala wa muda mrefu wa jeshi.
Alishinda tuzo ya Nobel mwaka 1991 kwa kupigia debe demokrasia nchini humo lakini aliachiliwa kutoka kifungo cha nyumbani mwaka 2010.
Chama chake cha National League for Democracy (NLD) kilishinda uchaguzi wa mwaka 2015 ulioandaliwa kama njia ya kuleta mabadiliko.
Kilishinda pia uchaguzi wa mwaka 2020 lakini jeshi likadai kwamba kulikuwa na udanganyifu na ndio maana lilinyakua mamlaka kwa madai ya kuchunguza udanganyifu huo.