Umoja wa Afrika, AU umetakiwa kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wajane barani Afrika.
Pendekezo hilo limetolewa na Mkewe Naibu wa Rais Dorcas Rigathi wakati akihutubia Kongamano la kwanza la Wajane barani Afrika lililoanza huko Zanzibar jana Alhamisi.
Pendekezo hilo sasa litazingatiwa na kujumuishwa kwenye mahitimisho ya mwisho yatakayoandaliwa mwishoni mwa kongamano hilo la siku tatu na kuwasilishwa kwa AU ili kuzingatiwa.
Bi. Dorcas pia ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kufanya mipango ya kuwaweka wajane katika vyama vya ushirika wa akiba na mikopo na mashirika ya kijamii ili kutumia vyema uwezo na ari yao ya ujasiriamali kukuza maendeleo barani humo.
“Barani Afrika, tuna ari ya ujasiriamali na wanawake ni wajasiriamali mno. Hebu AU ibuni sera ambapo wajane ni wahusika wakuu katika nyanja za biashara na uwekezaji,” alipendekeza Bi. Dorcas.
Katika hotuba yake, aliyekuwa Mama wa Taifa wa Tanzania Anne Mkapa alitambua changamoto wanazopitia wajane ikizingatiwa yeye binafsi alimpoteza mumewe, Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa mnamo mwaka 2020.
“Kuangazia masuala yanayowaathiri wajane barani Afrika kunahitaji mtazamo unaohusisha pande nyingi na wa wigo mpana ambao unaangazoa vyanzo vikuu vya ujane, na kuwawezesha wajane kufikia haki zao na rasilimali,” alisema Bi. Mkapa.
Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi alizungumzia masaibu ya wajane na kutoa wito kwa mataifa ya Afrika kuangazia kwa makini mateso yao na njia za kuwaondolea magumu wanayokumbana nayo maishani.
“Wajane wanapaswa kutambuliwa kisheria na kuheshimiwa, kuwezeshwa kiuchumi, na kupewa fursa zinazohitajika za kiafya na elimu. Ni jukumu letu kuhakikisha wajane hawanyanyaswi, hawadunishwi na kutumiwa vibaya,” alisema Rais Mwinyi.
Dkt. Mwinyi alifungua kongamano hilo ambalo pia lilihudhuriwa na Mkewe Mariam Mwinyi, Mkewe Rais wa Zimbabwe Auxillia Mnangagwa, Mkewe Rais wa zamani wa Zanzibar Mama Shadia Karume na Rais wa Umoja wa Wajane barani Afrika Hope Nwakwesi miongoni mwa wengine.
Wajane zaidi ya 800 wanahudhuria kongamano hilo kutoka mataifa ya Nigeria, Cameroon, Tanzania, Zanzibar, Kenya, Zimbabwe, Zambia, Uganda na Sierra Leone.