Umoja wa Afrika (AU) unapanga kupeleka ujumbe wa ngazi ya juu wa jopo la washauri mjini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, kushughulikia mgogoro unaoendelea nchini humo na kusababisha ukosefu wa usalama.
Taarifa iliyotolewa na AU imesema, jopo hilo litafanya majadiliano na wadau wote ili kuboresha juhudi za upatanishi na kuunga mkono utekelezaji kamili wa Makubaliano Yaliyohuishwa ya Mgogoro wa Sudan Kusini (A-ARCSS).
Taarifa hiyo imesema, Umoja wa Afrika unazitaka pande zote husika kudumisha mapendekezo ya makubaliano hayo, na kwamba umoja huo unaendelea kushirikiana na wenzi wa kikanda na kimataifa, ikiwemo Mamlaka ya Maendeleo ya Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Umoja wa Mataifa (UN) ili kuunga mkono mpito wa Sudan Kusini kuelekea amani ya kudumu na demokrasia.